
Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga, kwamba endapo atashindwa
kusimamia vema agizo la urasimishaji makazi holela na uandaaji wa hati miliki kwa
wananchi, atatumbuliwa.
Alitoa tahadhari hiyo juzi baada ya
kusomewa taarifa ya utekelezaji wa urasimishaji na uandaaji wa hati
za ardhi ambako Halmashauri ya Ilemela imetekeleza kwa asilimia moja kwa
kuandaa hati 834 huku viwanja vingine 16,000 vikiwa vimepimwa bila
kuandaliwa hati.
Lukuvi ambaye
alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa
kuandaliwa hati hizo ndani ya Halmashauri ya Ilemela
ambayo ina maofisa ardhi na watathmini zaidi ya 40 kmeisababishia
hasara Serikali.
Alisema kazi hiyo ingefanyika
ilivyotarajiwa serikali ingepata mapato ya Sh bilioni 2.5 kwa mwaka
lakini kilichopatikana ni Sh bilioni 1.3 tu.
“Hakuna halmashauri nchini iliyo na
watumishi wengi wa idara ya ardhi kama Ilemela na Nyamagana mara zote
nimekuwa nikifikiria kuwahamishia wilaya nyingine kama Geita kwa Mheshimiwa
Rais, Dk. John Magufuli ambako hakuna hata mmoja.
“Lakini leo pamoja na wingi
wenu mnaandaa hati 834 huku viwanja 16,000 mkishindwa kuvikamilisha kwa muda
niliotoa.
“Sasa Mkurugenzi nakuambia kwamba
Serikali imewavumilia vya kutosha na sasa kama hautabadilika kwa muda
ambao nimekuongezea kuanzia sasa hadi Juni 30, mwaka huu tambua kwamba
kitambi chako kitapata pancha.
“Wewe mwenyewe utajua namna ya
kuiziba pancha hiyo, hatuwezi kuimba wimbo huo huo kila mwaka.
“Kuna vitu vidogo vidogo vya
hapa halmashauri mnavifinyia kazi lakini suala ambalo ni la
muhimu mnashindwa kukamilisha.
“Nilikuwa namuona mkurugenzi ni
mjanja lakini anachokifanya hapa ni kama kutwanga maji kwenye kinu
kwa sababu kodi ya ardhi haikusanywi,” alisema.
Waziri alisema Halmashauri za
Ilemela na Nyamagana zinatakiwa zikamilishe hatua hiyo Juni 30,
mwaka huu atakapoifunga rasmi na kutangaza ‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza
ifikapo Agosti.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa
baada ya kufungwa urasimishaji makazi haitatokea
tena fursa ya namna hiyo.
Alisema wananchi ambao hawatakuwa
na hati ya eneo analoishi watahesabika kama wavamizi, hivyo watapoteza haki yao
na maeneo hayo yatachukuliwa na Serikali kwa shughuli nyingine.
Lukuvi alisema Serikali kuu
imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan ya Mwanza ambayo
itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu, kazi ambayo itafanywa na
wataalamu kutoka China.
No comments:
Post a Comment