
Shirikisho la Vyama Huru vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeitaka Serikali kuharakisha mchakato wa fao la
kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ili wafanyakazi wapate haki yao.
Limeitaka pia kuangalia upya makato
ya kodi ya mishahara ili yanufaishe watumishi wote na kueleza kuwa
kilichopunguzwa mwaka jana kinalinda wafanyakazi wachache wa kima cha chini cha
mishahara.
Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya
Msigwa, alisema hayo kwenye hotuba ya Shirikisho hilo mbele ya Rais John
Magufuli kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mjini
Moshi, Kilimanjaro jana.
Alisema kwa muda mrefu wafanyakazi
wamekuwa wakisubiri upitishwaji wa fao hilo ambalo litawasaidia kujikimu
wanapokosa ajira huku akiongeza kuwa kiwango cha kodi ya asilimia tisa
kinachotozwa kinanufaisha watumishi wa mshahara wa kima cha chini.
“Tunaiomba Serikali iharakishe
kuanzisha fao la kukosa ajira, ili linufaishe wafanyakazi. Kingine vikokoteo
vya mafao ya mifuko ya jamii viboreshwe ili watumishi waone matunda ya
kuchangia,” alisema Dk Msigwa.
Aliishauri Serikali kufanya
maboresho kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo kuunda mifuko miwili wa
umma na wa binafsi ili kuondoa mkanganyiko wa vikokoteo uliopo, wingi wa mifuko
ya hifadhi na kupunguza muda wa wastaafu kusotea mafao.
Alifafanua, kwamba baada ya
Serikali kupunguza kiwango cha kodi ya mishahara (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi
tisa, TUCTA imebaini wafanyakazi wanaopokea mishahara ya kima cha chini ndio
wanufaika wakubwa, huku wenye kima cha juu wakiendelea kubanwa.
Kuhusu wawekezaji, Dk Msigwa
alisema wapo wanaokiuka sheria za kazi na kanuni za ajira, ikiwamo kunyima
wafanyakazi haki ya kuunda vyama vya kutetea maslahi yao, pamoja ulipaji
mishahara kibaguzi.
Alibainisha kuwa wapo wawekezaji
wanaolipa watumishi wenye Shahada kutoka nje ya nchi Sh milioni saba na
kuwalipa wazawa Sh 700,000.
Aidha, aliiomba Serikali kuzifanyia
maboresho sheria za utumishi wa umma zinazohusu uhusiano wa kazi ili
ziwawezeshe kupeleka masuala yao kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya
Kazi (CMA).
Pia aliitaka Serikali kuwezesha
majaji kwenda mikoani kumaliza usikilizaji kesi za wafanyakazi kwa wakati na
haki itendeke huku akibainisha kuipunguzia majukumu Wizara ya Kazi, Ajira na
Watu Wenye Ulemavu ili ishughulikie matatizo ya wafanyakazi.
Alisema TUCTA inaipongeza Serikali
kwa kupambana na rushwa, ufisadi, kuondoa watumishi hewa, kupambana na dawa za
kulevya na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment