
Rais John Magufuli ametangaza
kuwa Serikali yake itatoa nyongeza ya mshahara ya mwaka na kupandisha madaraja
ya kazi kuanzia Bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2017/18.
Aidha, amepiga marufuku wafanyakazi
wa Serikali kuhamishwa kituo cha kazi bila kulipwa stahiki zake, akisema lengo
la hatua hiyo ni kuepusha madai yasiyo na sababu.
Rais Magufuli alisema hayo jana
kwenye sherehe za Sikukuu ya Mei Mosi zilizofanyika kitaifa Moshi mkoani
Kilimanjaro.
Alisema Serikali ililazimika
kufanya ukaguzi wa watumishi wake wote kabla ya kufanya uamuzi wowote kuhusu
maslahi ya wafanyakazi na kwamba baada ya kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti
vya kughushi atakaa na Baraza la Mawaziri kufanya maboresho.
“Acheni tufagie nyumba kwanza,
mlitaka nitangaze nyongeza huku wakiwamo watumishi hewa na wasio na vyeti? …
Mwaka huu tutapandisha madaraja ya kazi na kuweka nyongeza ya mishahara kuwa
sawa na madaraja stahiki ambayo yapo kisheria,” alisema.
Rais alisema mchakato wa kusafisha
watumishi wenye upungufu na hewa ulikuwa mgumu, hivyo ni wakati mwafaka kwa
ambao wanastahiki kupata promosheni kunufaika, kwani wangefanya kabla kundi la
wafanyakazi 19,000 waliondolewa lingekuwapo.
Magufuli alisema pamoja na kuongeza
mishahara na kupandisha vyeo, Serikali inatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi
52,000 ili kuziba mapengo mbalimbali katika utumishi wa umma.
“Mei Mosi si kwa ajili ya Tanzania
bali duniani kote. Ni siku ya kukumbushana na kutafakari mambo kuhusu
wafanyakazi na kutatua matatizo yanayowakabili, hivyo nimechukua changamoto
zenu na ninaahidi kuzifanyia kazi,” alisema.
Alipongeza viongozi wa Shirikisho
la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kwa kutambua dhamira ya Serikali, hivyo
kuwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha, alisema changamoto za
kisheria zinazowakabili wafanyakazi, waziri husika atazifikisha bungeni na
zikipitishwa atasaini muda huo huo.
“Nawahakikishia kuwa tunaanza
ukurasa mpya. Ndiyo maana mnaona hii siku ni tofauti. Serikali tumeamua
kuimarisha maslahi ya wafanyakazi. Na nyie muwe tayari kuchapa kazi,” alisema.
Rais Magufuli alisema wafanyakazi
ndio injini ya maendeleo katika Taifa lolote kubwa duniani, hivyo wanapaswa
kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Kuhusu fao la kazi, alisema
Serikali inalifanyia kazi na kuna mchakato unaendelea mfanyakazi anapoacha
ajira kabla ya kustaafu, alipwe sehemu ya mafao.
Akizungumzia bima, alisema Serikali
inaendelea na utaratibu wa kuanzisha fao la Bima ya Ajira na wadau wameshatoa
maoni, hivyo wakati ukifika watapewa taarifa rasmi.
Akijibu hoja ya uhuru wa
wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi, alisema suala hilo
lilishazungumzwa mwaka jana na lipo kwa mujibu wa sheria na hakuna mwajiri
aliye juu ya sheria.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli
ameziagiza wizara na taasisi kuunda mabaraza ya wafanyakazi kulingana na
mahitaji na kuwa kwa sasa yapo mabaraza 478.
Aidha, alitaka waajiri kutoa
mikataba ya ajira kwani ni jambo la kisheria na si hiari.
Akijibu madai ya wafanyakazi baada
ya kuhamishwa eneo la kazi, Rais aliwataka wafanyakazi kutohama eneo bila
kulipwa stahiki zao, kwani ni kinyume na sheria.
Rais Magufuli alisema hakuna sababu
ya mfanyakazi kuhamishwa bila kulipwa, kwani kinachoendelea ni lawama kwa
Serikali, jambo ambalo hataki kulisikia tena.
Aidha, kuhusu mfumuko wa bei, Rais
alisema Serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha hali hiyo inadhibitika, huku
akibainisha kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zitafanikisha mchakato huo.
Halikadhalika Rais alisisitiza kuwa
Serikali ina mpango wa kuboresha na kufufua viwanda hali ambayo itachangia
kuongezeka kwa ajira.
Alisema kupitia mifuko ya hifadhi
ya jamii jumla ya dola za Marekani milioni 156 zitatumika kujenga viwanda
nchini.
No comments:
Post a Comment