
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, imemtaka Gavana wa Benki Kuu (BoT) Benno Ndulu, na Mwendeshaji wa benki
ya FBME, Lawrence Mafuru, wafike mahakamani kujieleza jinsi watakavyotekeleza
amri iliyoitaka BoT kulipa Sh bilioni 92.
Maofisa hao wanatakiwa kuieleza
mahakama watakavyoilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo na kama
watashindwa kufanya hivyo, watafungwa jela kama wafungwa wa kesi ya madai.
Utekelezaji wa amri hiyo unatokana
na uamuzi wa shauri namba 129 la mwaka 2009, ulioiamuru benki ya FBME kuilipa
kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo baada ya kukamata kiwanda chake na
kukiuza kwa kampuni ya Five Star Investment ltd.
Uuzwaji wa kiwanda hicho ulitokana
na mgogoro wa ulipaji mkopo ambao kampuni ya Coast iliuchukua katika benki
hiyo.
BoT inahusishwa kwenye shauri hilo
kutokana na kuchukua uendeshaji wa benki ya FBME baada ya benki hiyo kuhusishwa
na utakatishaji fedha nchini Cyprus.
Maofisa hao walitakiwa kufika
mahakamani hapo Septemba 16 mwaka huu kwa ajili ya kueleza jinsi
watakavyotekeleza amri hiyo, lakini hawakufika kwa kuwa wamewasilisha maombi ya
kusimamisha shauri hilo ambayo yamepangwa kusikilizwa leo mbele ya Jaji Ama
Munisi.
Katika kesi ya msingi
iliyofunguliwa na kampuni ya Coast, mahakama iliamuru FBME iilipe kampuni hiyo
Sh bilioni 21.2 na riba ya asilimia 21 kwa mwaka tangu Juni 28, 2001 hadi
hukumu ilipotolewa, Julai 27, 2015.
Baada ya uamuzi huo, walalamikaji
walipeleka maombi ya utekelezwaji wa hukumu hiyo, ambayo ukijumlisha na riba ni
sawa na Sh bilioni 92.2.
Kutokana na maombi hayo, mahakama
ilimuelekeza Gavana wa BoT kukamata akaunti mbili zinazomilikiwa na benki ya
FBME, hata hivyo BoT iliwasilisha maombi ya kuchunguzwa kwa umiliki halali wa
akaunti zinazoshikiliwa na kuiomba mahakama isitishe amri hiyo kwa kuwa BoT
siyo miongoni mwa walalamikiwa kwenye shauri la msingi.
BoT iliingilia kati suala hilo, kwa
kuwa kwa sasa ndiyo inayosimamia uendeshwaji wa benki ya FBME kwa ajili ya
kulinda amana za wateja baada ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha.
Baada ya kusikiliza maombi hayo,
mahakama iliondoa amri hiyo na kuamuru benki hiyo ilipe fedha, hata hivyo
walalamikaji waliwasilisha maombi mengine ya kukazia hukumu katika Mahakama
Kuu.
Katika maombi hayo Msajili wa
Mahakama Kuu, Projest Kahyoza alitoa siku saba kwa maofisa hao kufika
mahakamani kujieleza jinsi watakavyolipa fedha hizo na wakishindwa watafungwa
jela kama wafungwa wa madai.
No comments:
Post a Comment