
Kampuni ya Kufua Umeme ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imegeuziwa kibao katika suala la
Escrow, imefahamika.
Kampuni hiyo imetakiwa kurejesha
zaidi ya Dola za Marekani milioni 100 (Sh bilioni 216.2 ) kwa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zikiwa fedha za ziada
ambazo ililipwa kabla ya hesabu kufanywa upya.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Biashara uliotolewa Septemba 12 mwaka
huu unaoitaka Tanesco kuilipa Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani
milioni 148.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo
kutokana na kesi iliyofunguliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong
(SCB-HK) dhidi ya Tanesco ikidai kulipwa Dola za Marekani milioni 369.
Kwa mujibu wa Wakili wa Tanesco,
Richard Rweyongeza, amesema walichokuwa wanabishania mahakamani si Tanesco
kulipa bali walikuwa wanabishania shirika hilo litalipa kiasi gani na linamlipa
nani.
“Kabla hatujaingia katika kutetea
kesi hiyo, mwaka 2014 mahakama hiyo ilisema inayo madaraka na ikaamuru Tanesco
kuilipa SCB-HK.
“Sisi tuliingia kutetea baada ya
uamuzi huo, Mei, 2014 tukaomba hesabu zifanyike upya kwa malekezo
yaliyotolewa na mahakama hiyo kujua deni halisi.
“Hesabu zilipofanyika kwa mtaji wa
mwekezaji, walichukua mkopo wakahesabu kuwa ni mtaji, hatua hiyo ilikataliwa na
mahakama.
“Kabla ya hesabu kufanyika ndipo
likaingia suala la akaunti ya Tegeta Escrow. Fedha zilipochukuliwa katika
akaunti hiyo, SCB-HK wakabadilika wakasema hakuna haja ya kufanya hesabu upya
kwa sababu Tanesco wamekubali viwango hivyo ndiyo sababu waliwalipa IPTL.
“Tulibishania hoja hiyo ya kulipa
kwa viwango vya zamani ikaamuriwa hesabu zifanyike upya, mahakama ilikubali
hesabu ifanyike kwa kutumia mkopo wa wana hisa.
“Baada ya kuamuru hivyo, deni
likashuka kutoka walichokuwa wakidai Dola za Marekani milioni 369 hadi
kuamuriwa kulipa Dola za Marekani milioni 148,”anasema Wakili
Rweyongeza.
Alisema IPTL walilipwa Dola za
Marekani milioni 246 kwa kutumia viwango vya zamani na kwamba uamuzi uliotolewa
unaanza kutumika katika kipindi chote ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa mpaka
mwaka 2015.
“Kutokana na hesabu hizo gharama
ilikuwa chini, IPTL ililipwa zaidi hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani
zaidi ya milioni 100 kwa Tanesco,”alisema.
Rweyongeza alisema walipendekeza
SCB-HK wadai fedha zao kwa IPTL lakini mahakama hiyo ilikataa na kuamuru
Tanesco ndiyo walipe hivyo kwa mtazamo wa kawaida IPTL inatakiwa kurejesha
fedha kwa shirika hilo.
Katika kuhitimisha, mahakama hiyo
ilisema pande zote mbili zinazopingana zilishinda katika maeneo muhimu
waliyokuwa wakibishania lakini zilipoteza katika hoja nyingine.
Baada ya kumaliza kusikiliza kesi
hiyo mahakama iliamuru pande hizo mbili kulipa gharama za usuluhishi na
nyingine kwa viwango sawa.
Malipo hayo na anayelipwa katika
mabano ni Dola za Marekani 254,775.02 (Profesa MC Rae), Dola 171,278.36
(Profesa Douglas) na Dola 370,126.76 kwa ajili ya Profesa Stem.
Gharama nyingine zilizokadiriwa
moja kwa moja ni Dola za Marekani 157,336.26 na gharama za utawala kwa mahakama
hiyo Dola za Marekani 180,000 ambako jumla ya gharama zote wanazotakiwa kulipa
Tanesco na SCB-HK ni Dola za Marekani 1,133,516.42.
Hata hivyo Rweyongeza alisema
pamoja na ushindi huo hawakuridhishwa na uamuzi huo kwa sababu katika uamuzi wa
kwanza, mahakama hiyo ilikataa hesabu kupigwa kwa kutumia kiwango cha 22.31
lakini bado katika uamuzi huu walitumia kiwango hicho kufanya hesabu hivyo
walikosea kufanya hivyo.
Hoja ya pili, alisema SCB-HK si
mwekezaji hivyo hakustahili kupeleka kesi hiyo mahakamani na kwamba hapakuwa na
hoja.
“Sababu nyingine ya kutoridhishwa
na uamuzi huo ni kwamba hatukupewa nafasi ya kujibu hoja mpya zilizowasilishwa
kuhusu Tanesco kwamba ilidanganya, tulipaswa kujibu kwa maelezo ya mashahidi si
mawakili.
“Tuliwasilisha hoja kwa maandishi,
zilipotokea hoja mpya tulitakiwa kuzijibu kwa kuleta mashahidi, tunapinga pia
uamuzi ulioitambua SCB-HK kuwa ilistahili kisheria,”alisena
Rweyongeza.
Suala hilo limeibuka ikiwa imepita
miaka mitatu tangu Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali na viongozi wa
Wizara ya Nishati na Madini kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Dola za Marekani
milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni 300) kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Fedha hizo zilitolewa na kwenda kwa
mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP),
Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake nchini na Afrika Kusini.
Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa
inawakilishwa na mawakili wa kampuni za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax
Law Partners.
Chanzo cha Escrow
Mwanzoni mwa miaka ya 1990
nchi ilikuwa na upungufu wa umeme kutokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa,
ambapo 1994 serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa IPTL ilikuwa iliyokuwa
ikimilikiwa na VIP ya Tanzania iliyokuwa na asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia
yenye asilimia 70.
Tanesco na IPTL walisainiana
mkataba wa miaka 20, hata hivyo uzalishaji haukuanza mara moja kutokana na
mgogoro ulioibuka baina yao (Tanesco na IPTL) .
Mwaka 2002 IPTL ilianza
kuzalisha umeme na mkataba ukaanza kuhesabiwa hapo, lakini kutokana na mgogoro
ikafunguliwa akaunti ya Escrow na mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri kupinga
tozo la Capacity Charge
Uwiano wa mtaji ni 70 kwa 30 na
uamuzi haujabadilishwa na mahakama yoyote. Mwaka 2004 Kampuni ya Mkono
& CO advocates iliishauri Tanesco iendelee kupinga Capacity Charge
London.
Inaelezwa kuwa Agosti 2005, benki
ya SCB-HK ilinunua kwa bei ya punguzo ya dola za Marekani 76.1 kutoka Benki ya
Malaysia ya Danaharta baada ya kushindwa kurejesha deni la muda mrefu kutoka
IPTL.
Bei halisi ya deni hilo ilikuwa ni
dola milioni 101.7 kwa mujibu wa ushahidi uliopo ambako IPTL ilikopa dola
milioni 100 mwaka 1998 kutoka kwa mbia wa benki ya Malaysia ili kujenga mtambo
wa kufua umeme wa megawati 100 wa Tegeta.
Kwa mujibu wa makubaliano
hayo, SCB-HK ilipewa kandarasi kadhaa ikiwamo haki ya kulipwa deni la 1997,
ambako mkataba wa utekelezaji na hatia ya makubaliano ya dhamana
iliyosainiwa kati ya IPTL na Serikali.
Fedha zilivyotolewa
Akaunti ya Tegeta Escrow
ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuhifadhi fedha za malipo ya tozo
ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na Kampuni ya
IPTL na suala hilo lilipelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa masharti ya
uendeshaji wa akaunti ya Escrow, fedha zilitakiwa zitolewe baada ya Mahakama
kutoa uamuzi wa mgogoro huo, lakini wakati ilitaka pande hizo mbili zikutane na
kukokotoa viwango vya tozo, fedha hizo zilitolewa na kulipwa mmiliki wa Kampuni
ya Pan Africa Power Solution (PAP) jambo lililosababisha kuibuka kashfa
hiyo.
Ilivyotua bungeni
Aliyekuwa wa kwanza kulifikisha
bungeni suala hilo ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ambaye
aliwalipua baadhi ya mawaziri wa Serikali ya awamu ya nne kuhusika na mpango
huo.
Hatua hiyo ilisababisha Spika wa
Bunge la 10 kuagiza uchunguzi wa vyombo vya dola kuweza kuchimbua kwa
undani wizi huo.
Baada ya kukamilika ilikabidhiwa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAP) chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake
Zitto Kabwe na Makamu wake, marehemu Deo Filikunjombe.
Novemba 28 mwaka 2014, Bunge
la 10 lilitoa maazimio manane kuhusu suala hilo huku Harbinder Singh
Sethi, James Rugemalira wa (VIP), aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati
na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Shirika la Umeme wa Umeme Tanzania (TANESCO) walionekana kuhusika kwa namna
moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za
Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda Pan African Power Solutions Ltd (PAP) na
VIP.
Bunge pia liliazimia mawaziri wa
wakati huo wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Fredrick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa
kati huo, Eliachim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO
wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Mawaziri hao walipoteza nyadhifa
zao huku Profesa Muhongo akijiuzulu na Tibaijuka uteuzi wake ukifutwa na Rais
wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Chanzo Mtanzania
No comments:
Post a Comment