
WATU 13 wamefariki dunia katika
ajali iliyohusisha basi la Super Shem lenye namba za usajili T 874 CWE
lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Mwanza na Hiace yenye namba T 368 CWQ
iliyokuwa ikitoka Jijini Mwanza kuelekea Wilaya ya Kwimba.
Katika ajali hiyo mfanyabaishara
ndogo ndogo maarufu machinga, Peter Tobari, aliokoa maisha ya abiria zaidi ya
30 na kumsaidia dereva wa basi la Super Shem ambaye alikuwa amekandamizwa miguu
na basi hilo baada ya kugongana na Hiace.
Ajali hiyo imetokea siku mbili
baada ya ile ya basi la Kampuni ya New force iliyotokea mkoani Njombe
ikihusisha basi lenye namba T 429 DEU lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda
Songea mkoani Ruvuma, ambapo watu 12 walifariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa
vibaya. Katika ajali ya Mwanza, gari dogo aina ya Hiace liligongana uso kwa uso
na basi la Super Shem na kusababisha vifo hivyo na wengine 10 kujeruhi.
Ajali hiyo imetokea umbali wa mita
200 kutoka kituo kidogo cha mabasi cha Hungumalwa njia panda ya Shelui na
Mwamashimba katika Kijiji cha Mwamaya wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ilielezwa
katika tukio hilo, dereva wa Hiace aliingia barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga
bila kuchukua hadhari na hivyo kukutana na basi hilo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali
hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya ajali
hiyo watu 10 walikufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa, ambapo mmoja
alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wawili
walifariki dunia wakati wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa
matibabu zaidi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Wilaya ya Kwimba, Dk. Bethod Nchemba, akizungumzia ajali hiyo alisema
walipokea majeruhi 10 wakiwemo wanaume na wanawake watano ambapo
mmmoja alikuwa na hali mbaya na alifariki akiwa mapokezi wakati
akiendelea kupewa huduma.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni
Monica Shija, Christina Costantine, Theresia Majenga wote wakiwa wakazi wa
Kijiji cha Gulumwa wilayani Kwimba, Lwinzi Kope mkazi wa Kijiji cha Chaselwe,
Mabula Magi wa Rukwa, Isaya Deogratius mkazi wa Mbande, Moses Kamel wa Kijiji
cha Bupamwadomu, George Ndila mkazi wa Sangu, Kondakta wa hiace aliyefahamika
kwa jina moja la Poni pamoja na mtu mmoja mwanaume, mama mmoja na mtoto ambao
hawajafahamika wote wakiwa ni abira wa Hiace.
Alisema majeruhi watatu
wanaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo na miili tisa kati ya 11
imeshatambuliwa isipokuwa mwili wa mama mmoja na mtoto anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka 5 na majeruhi sita wamelazimika kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment