Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bw. Evarist Ndikilo atoe wiki mbili kwa wakuu
wa taasisi za umma na za binafsi wajieleze ni lini wataendeleza viwanja vya
ofisi walivyopewa mjini Kibaha.
Ametoa agizo hilo jana Septemba 21,
2016 wakati akizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015 – 2020) na
Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, Kibaha, mkoani Pwani.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo kwamba kuna taasisi za umma
na za binafsi ambazo zimepewa viwanja vya kujenga Ofisi kwa zaidi ya miaka
mitatu lakini zimeshindwa kuviendeleza hadi sasa wakati kuna watu bado wana
shida ya kupatiwa viwanja.
“Kibaha ni kimbilio la mkoa wa Dar
es Salaam, kule kumejaa na hapa kuna nafasi kwa hiyo hawa ambao hawajaendeleza
waandikie barua leo hii hii na uwape wiki mbili waeleze ni lini watakuwa tayari
kuanza kazi hiyo.” – Majaliwa
Taasisi hizo zilizotanjwa na Waziri
Mkuu ni Hazina ndogo yenye viwanja viwili ambapo kiwanja kimoja chenye namba
232 kimeendelezwa lakini kiwanja kingine chenye namba 221 bado hakijaendelezwa.
Taasisi nyingine na viwanja
vyao kwenye mabano ni Chuo Kikuu Huria (kitalu na. 228), Njuweni Institute
(kitalu na. 229), TANESCO (kitalu na. 218), TRA (kitalu na. 233) na SF Group
(kitalu na. 225). Vingine ni vya Benki ya CRDB na TAKUKURU ambavyo hakutaja
namba za vitalu vyake.
Majaliwa alisema kuwa anajua kuna
watu wa Serikali watasema hawana bajeti, lakini Bunge la bajeti linaanza Aprili
mwakani. Kwa hiyo, wajipange kwenye bajeti ijayo, ili ifikapo Julai mosi, 2018
hawajafanya kitu, wachukuliwe hatua.
“Tuchukue viwanja vyetu tuwape
wengine, na hawa wanaosuasua, tuwaache ili watakapokuwa tayari waombe upya na
tutawapa wakati mwingine,” Majaliwa.
Waziri Mkuu pia alimtaka Ndikilo
awawekee deadline ya kujieleza katika barua hizo.
No comments:
Post a Comment