Kiongozi huyo amesema Bw Obama anaweza "kwenda
jehanamu".
Umoja wa Ulaya, ambao pia umemkosoa Bw Duterte, unaweza
"kuchagua kwenda eneo la kutakasia dhambi ndogo, kwa sababu jehanamu
kumejaa", amesema.
Watu karibu 3,000 wameuawa tangu kiongozi huyo alipoingia
madarakani mwezi Juni.
Watu wanaoshukiwa kulangua mihadarati au kuwa waraibu wa dawa
hizo wamekuwa wakiuawa na maafisa wa polisi na magenge yanayoungwa mkono na serikali.
Bw Duterte amesema Urusi na China wako tayari kuwa washirika
wake.
Wanajeshi wa Ufilipino na Marekani kwa sasa wanafanya mazoezi ya
pamoja ya kijeshi lakini Bw Duterte amesema mazoezi hayo hayana manufaa kwa
raia wa Ufilipino.
Msemaji wa ikulu ya White House Josh Earnest amesema Washington
kufikia sasa haijapokea ombi lolote rasmi kutoka kwa Ufilipino kufanyia
marekebisho mikataba ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Akiwahutubia maafisa wa serikali na wafanyabiashara, Bw Duterte
amesema amesikitishwa sana na Marekani kwa kukosoa mbinu za Ufilipino za
kukabiliana na mihadarati.
Ameeleza Marekani kama mshirika asiye wa kutegemewa.
"Badala ya kutusaidia, wizara ya mambo ya nje (ya Marekani)
ndio wa kwanza kutukosoa, kwa hivyo wanaweza kwenda jehanamu, Bw Obama, unaweza
kwenda jehanamu."
Baadaye Jumanne, alitahadharisha kwamba: "Mwishowe huenda,
nikiwa bado uongozini, nikajitenga na Marekani. Heri kwenda kwa Urusi au Uchina."
Aidha, Bw Duterte amefichua kwamba Marekani imekataa kiuzia
silaha serikali yake lakini akaongeza kwamba watazinunua kwingine.
"Iwapo hamtaki kuuza silaha, nitaenda Urusi. Niliwatuma
majenerali Urusi na Urusi walisema, 'Msiwe na wasiwasi, tuna kila kitu mnachohitaji,
tutawapa'.
"Kuhusu China, walisema, 'Njooni na mtie saini na kila kitu
kitafikishwa kwenu'," Rais Duterte amesema.
Ufilipino ilikuwa koloni ya Marekani na imekuwa mshirika mkuu
Asia mashariki.
Wanajeshi 1,100 wa Marekani na 400 wa Ufilipino wanashriiki
mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ambayo yataendelea kwa siku nane.
Uhusiano baina ya Marekani na
Ufilipino ulidorora mwezi uliopita baada ya Rais Duterte kuonekana kumtusi Rais
Obama.
No comments:
Post a Comment